Kidonda cha Upasuaji wa Uzazi Kutopona!
Kidonda cha Upasuaji wa Uzazi ni Kidonda ambacho hutokea baada ya kukatwa kwa tumbo sehemu ya chini ya Kitovu kwa ajili kutoa Mtoto kutoka kwa mjamzito endapo mjamzito ameshindwa kujifungua kwa njia ya kawaida (Uzazi wa kawaida), Kidonda cha kwenye ngozi sehemu ya chini ya tumbo lako baada ya kujifungua kwa upasuaji hutakiwa kupona mapema sana mara baada ya kujifungua kwa njia hii ya upasuaji.
Kidonda cha kwenye ngozi hutakiwa kupona kati ya siku ya 7 hadi siku ya 10 tokea kujifungua kwako kwa upasuaji, Endapo kidonda hicho kitachelewa kupona kwa namna yoyote ile au kuanza kuonesha dalili za maambukizi huweza kuwa na athari katika afya yako baada ya Kujifungua.
Maambukizi ya Vijidudu (Bakteria) kwenye kidonda au mshono wa upasuaji ni pale ambapo mara baada ya mama kujifungua kwa upasuaji kidonda huanza kuonesha dalili hatarishi na kuchelewa kupona kuliko kawaida zaidi ya wiki 2, kitalaam huitwa Surgical site infection (SSI).
Hali hii huweza kuathiri kati ya akina mama wawili (2) hadi saba (7) kati ya 100 waliojifungua kwa njia hii ya upasuaji, Kwa kawaida dalili za maambukizi ya vijidudu huanza kuonekena kati ya siku 4 hadi 7 tokea kujifungua kwa upasuaji ijapokuwa baadhi ya Vijidudu ambao wameambukiza kwenye kidonda huweza kuonesha dalili baada ya masaa 48 (Siku 2) tokea kujifungua kwa upasuaji.
VIHATARISHI VYA MAAMBUKIZI KWENYE KIDONDA CHA UPASUAJI WA UZAZI.
Yako mambo mengi yanayoweza kukuhatarisha Mama uliyejifungua kwa upasuaji au kama una mpango wa kujifungua kwa upasuaji kuishia kuwa na maambukizi ya Vijidudu kwenye Kidonda (Mshono) cha upasuaji wa uzazi.
Vihatarishi hivyo inawezeka unavyo kabla ya kujifungua haswa kipindi cha Ujauzito yaani kabla ya kujifungua au baada ya kujifungua kwa upasuaji,Mambo yafuatayo yanaweza kukuhatarisha baada ya kujifungua kwa upasuaji ukaishia kuwa na maambukizi ya Vijidudu kwenye kidonda chako ambayo ni kama;
- Damu kuvilia katikati ya Kidonda (Mshono) cha Uzazi, Baada ya kufanyiwa upasuaji endapo damu ilivilia katikati ya Kidonda au mshono huweza kupata maambukizi ya vijidudu na kuwa kuhatarisha kidonda chako kupata maambukizi ya Vijidudu au bakteria.
- Aina ya mshono, Mama uliyejifungua kwa upasuaji mshono wa ulalo unauwezekano mkubwa wa kupata maambukizi kwenye kidonda haswa kama una Kitambi, umejifungua Mapacha kuliko mama aliyekuwa na mshono wa wima.
- Uzito mkubwa kupindukia (Kiriba Tumbo), Mama ukiwa na uzito mkubwa au kitambi wakati wa upausaji kidonda chako huweza kuwa na mafuta mengi endapo yasiposhonwa vizuri huweza kutengeza mazingira mazuri kwa ukuaji wa Vijidudu na kuambukiza kidonda chako.
- Maambukizi ya Kuta zinazomzunguka mtoto tumboni mwako, Kabla ya mjamzito kujifungua endapo kuna sababu fulani ilikupelekea ukapata maambukizi ya vijidudu kwenye kuta zinazomzunguka mtoto tumboni huweza kuongeza hatari ya kupata maambukizi ya kidonda cha ngozi yako.
- Kuto tumia dawa kinga kabla ya Upasuaji, Mjamzito endapo hujapata dawa kinga dhidi ya Vijidudud kabla ya kuingia kwenye chumba cha upasuaji, huweza kuongeza hatari ya kupata maambukizi kwenye kidonda cha upasuaji.
- Uchungu wa muda mrefu, Uchungu zaidi ya masaa 12 huweza kuchangia mama upate maambukizi kwenye kidonda chako baada ya kujifungua kwa upasuaji.
- Chupa kupasuka kabla ya Uchungu kuanza, Endapo ulipata shida ya chupa kupasuka kabla ya uchungu halafu ukafanyiwa upasuaji inawezekana kuhatarisha kidonda chako kupata maambukizi ya Vijidudu.
- Ugonjwa wa Kisukari katika Ujauzito, Inawezekana una ugonjwa wa kisukari wa muda mrefu (Kisukari aina ya 1, 2) au Kisukari cha Ujazito huweza kupelekea kinga ya mwili wako kushuka sana na unakuwa kwenye hatari ya kupata maambukizi kwenye kidonda cha upasuaji.
- Kujifungua kwa upasuaji wa dharura.
- Kujifungua kwa upasuaji mimba ya Mapacha, Mama ukiwa na Mimba ya mapacha tumbo huwa kubwa sana baada ya kujifungua inawezeka kuhatarisha kuishia kuwa na maambukizi ya kidonda cha upasuaji wako.
- Kujifungua kwa mara ya kwanza haswa njia hii ya upasuaji.
- Matumizi ya dawa za kupunguza kinga (Corticosteroids) mfano kama; Prednisolone kipindi cha ujauzito au baada ya kujifungua kwa upasuaji.
- Uvutaji sigara kwa Mjamzito au Mama unaishi na mumeo anavuta sigara huweza kuchangia kidonda chako kupata maambukizi.
SABABU ZA MAAMBUKIZI YA VIJIDUDU KWENYE KIDONDA CHA UPASUAJI WA UZAZI.
Pamoja na vihatarishi vingi tajwa hapo juu, yako ambayo mama uliyejifungua kwa upasuaji ukifanya yanaweza kupelekea au kusababisha moja kwa moja ukapata maambukizi ya Vijidudu kwenye kidonda cha upasuaji wako, Sababu hizo ni kama hizi;
- Kutozingatia usafi wa mwili na kidonda, Endapo umejifungua kwa upasuaji ila husafishi kidonda kulingana na maelekezo ya mhudumu wa afya aliyekuona kidonda lazima kipate maambukizi ya Vijidudu.
- Kuloanisha kidonda, Baada ya kujifungua kwa upasuaji endapo kwa namna yoyote kidonda chako kitakuwa kwenye unyevu basi kinaweza kupata maambukizi ya Vijidudu.
- Kutomaliza dozi ya dawa za kuua Vijidudu unazopewa hospitali.
- Uvivu wa kufanya mazoezi muda mfupi baada ya kujifungua kwa upasuaji na kuruhusiwa na mhudumu wa afya anayekuhamasisha kufanya mazoezi.
- Kuoga mapema kabla ya muda ambapo kidonda kupona na pasipokuwa na vitu vya kuzuia kidonda chako kuloana na maji.
- Kutotumia dawa vizuri za magonjwa mengine mfano; Dawa za ugonjwa wa kisukari aina 1 & 2 endapo ulikuwa muathirika wa ugonjwa huu na umejifungua kwa upasuaji.
FANYA MAMBO HAYA KUEPUKA MAAMBUKIZI YA KIDONDA CHA UPASUAJI WA UZAZI
Mama uliyejifungua kwa upasuaji ni vema kuzingatia mambo haya ili kujiepusha na maambukizi ya Vijidudu kwenye kidonda cha upasuaji wa uzazi au mshono mara baada ya kujifungua kwa upasuaji,mambo hayo ni kama;
- Usafi wa mwili na kidonda, Safisha kidonda chako baada ya kuruhusiwa hospitali kila baada ya siku 1 au kila siku kulingana na maelekezo ya mhudumu wa afya wako mpaka kidonda kitakavyo pona kabisa.
- Ukavu wa kidonda muda wote, Usiloanishe kidonda chako mapema kabla ya kupona, kama huna njia za kuweza kuzuia maji yasiingie kwenye kidonda ni bora usioge mpaka upone kidonda chako.
- Mazoezi ya kutembea tembea baada ya upasuaji, Mara baada ya kujifungua kwa upasuaji ndani ya masaa 24 anza kufanya mazoezi ya kutembea tembea.
- Kula mlo kamili ambao wenye protini nyingi kiasi ili uweze kupona kwa haraka zaidi.
- Kunywa maji lita 2 na nusu kila siku.
- Maliza dozi za dawa za kuua vijidudu kama ulivyoelekezwa na mhudumu wako, kwa kawaida dozi huwa ya siku 5 hadi 7 au zaidi kulingana na hali yako.
- Nyonyesha mtoto wako mchanga ipasavyo bila kusahau vyakula vya kuongeza maziwa kipindi chako cha mwanzoni cha kunyonyesha.
Response to "Kidonda cha Upasuaji wa Uzazi Kutopona!"
Je ikiwa nimejifungua kwa upasuaji mara tatu mfululizo,watoto wamepishana miaka miwili miwili,nikibeba ujauzito mwingine kuna hatari?
Message whatsApp namba +255 629 019 936