Vyakula Muhimu Kwa Mama aliyejifungua kwa Upasuaji!
Kujifungua kwa Upasuaji (Caesarean delivery) ni upasuaji mkubwa kama upasuaji mwingine wa Tumbo, japokuwa wakati mwingine utumbo huweza kuguswa wakati wa upasuaji huu ila ni mara chache sana. Hivyo Mama aliyejifungua kwa upasuaji huhitaji kutumia vyakula kwa ufasaha ili kuepuka changamoto za Kujifungua kwa upasuaji mfano; Kupata choo kigumu/Funga choo, Tumbo kujaa gesi, Kidonga kutopona kwa wakati na Kukosa Maziwa ya Mtoto wake na kushindwa kunyonyesha.
Ili kuepuka changamoto zinazoweza kutokea ndani ya wiki 1 hadi 2 tokea kujifungua mtoto kwa upasuaji, Mama aliyejifungua kwa upasuaji anapaswa kutumia vyakula stahiki na kuepuka baadhi ya vyakula vinavyoweza kuathiri afya yake mara baada ya kujifungua kwa upasuaji.
VYAKULA MUHIMU KWA MAMA ALIYEJIFUNGUA KWA UPASUAJI.
Vyakula vifuatavyo ni muhimu kutumiwa na Mama aliyejifungua kwa upasuaji ndani ya wiki 1 hadi 2 tokea kujifungua kwa upasuaji, ni muhimu Mama kutumia vyakula hivi ili kuepuka changamoto mbalimbali tajwa hapo juu kama; Kupata choo kigumu, Tumbo kujaa gesi, Kukosa Maziwa ya Mtoto mchanga na Kidonga kutopona kwa wakati na nk, Vyakula hivyo ni kama;
- Vyakula vyenye protini kwa wingi, Protini ni muhimu sana katika kujenga mwili na kukuza tishu za mwili hivyo Mama aliyefanyiwa upasuaji ili tishu zilizopo kwenye mshono kuweza kukua vizuri na Kidonda kupona kwa wakati huhitaji protini nyingi hivyo, Mama aliyejifungua kwa upasuaji huhitaji protini ya kutosha ili kukidhi mahitaji ya mwili wake, vyakula vye protini kwa wingi ni kama; Mayai, Nyama nyekundu (Nyama za Ng’ombe,Mbuzi,Kondoo na nk), Nyama za Ndege (Kuku,Bata na nk) Samaki (Sato,Saratoga,Pelege,Kambale,Sangara,kibua,mgebuka na nk), Maziwa na nk.
- Vyakula vyenye Nyuzi nyuzi, Vyakula vyenye nyuzi ni muhimu sana kwa Mama aliyejifungua kwa Upasuaji husaidia kuweza kupunguza changamoto za kupata choo kigumu kwa Mama, Vyakula vyenye nyuzi ni kama Mboga za Majani (Mchicha,Spinachi,Chainizi, Tembele, Figili, Majani ya Maboga na nk), Matunda (Papai,Parachichi,Embe,Nanasi,Epo na nk), Mikate ya Unga usiokobolewa na nk
- Maji ya Kunywa ya Kutosha, Tunaposema Maji ya kunywa ya kutosha kwa Mama aliyejifungua kwa Upasuaji tuna maanisha kunywa maji kuanzia lita 2 au zaidi kila siku au ndani ya masaa 24, Maji humsaidia Mama aliyejifungua, kupunguza shida za kuwa na choo kigumu na vile vile husaidia kutengeneza maziwa ya kichanga, Maji ni lazima yawe safi na salama ili kuepuka magonjwa mengine ambukizi endapo Mama atatumia maji yasiyo safi na salama.
- Vyakula vya Kuongeza Maziwa, Baada ya Kujifungu kwa Upasuaji baadhi ya akina mama hupata changamoto ya uhaba wa maziwa kwa ajili ya vichanga wao, hivyo ni vema kuhakikisha unapotumia vyukula vyako unaongeza na unga wa mbegu za maboga au unga wa mbegu za pilipili manga kwenye mchuzi wa samaki au nyama, vile vile unaweza kuweka unga huo kwenye mtori, uji au hata kwenye chai endapo unatumia pilipili manga.
- Wanga na Mafuta kiasi, Mama aliyejifungua kwa upasuaji anaweza kutumia vyakula vyenye wanga kwa kiasi kidogo,Si vema kutumia wanga mwingi huweza kupelekea ukosefu wa maziwa na pia kupelekea kupata choo kigumu katika kipindi cha ndani ya wiki 2 tokea kujifungua, hivyo Mama anapaswa kutumia kiwango kidogo cha Ugali,Wali au Uji wa ulezi vile vile ni vema kutumia mafuta na wanga kwa kiwango cha wastani haswa kama una uzito mkubwa.
- Madini na Vitamini mbalimbali,Mama aliyejifungua kwa upasuaji ni vema kuweza kupata madini mbalimbali ikiwemo madini chuma kwa ajili ya kumuongezea damu, hii ni kwa sababu Mama aliyejifungua kwa upasuaji hupoteza damu nyingi zaidi ukilinganisha na Mama aliyejifungua kwa njia ya kawaida, pia huhitaji madini mengineyo kama Magneziamu,Zinki,Potasiamu,Kalsiamu kwa ajili ya kuimalisha afya ya mwili wake, vile vile huhitaji vitamini mbalimbali kama vitamini D, Vitamini C, Vitamini A, Vitamini B (B1,B2,B3,B5,B9,B12), Vitamini E na nk ili kuhakikisha kuwa ana kinga bora ya mwili wake na kuwa na afya njema yeye pamoja na Mtoto anayenyonyesha,Vitamini hizi na Madini huweza kupatikana kwenye vyakula mbalimbali ikiwemo Maziwa,mboga mboga na matunda mbalimbali, japokuwa Mama anaweza kutumia dawa lishe kama pregnacare au prenatal vitamins kupata vitamini na madini hayo.
KUMBUKA: Mama aliyejifungua kwa upasuaji haruhusiwi kutumia vyakula au vinywaji kama Mikate ya unga uliokobolewa kama skonsi,Makande,Mboga jamii ya kabeji, Mapera, Wanga mwingi,Energy drinks,Pombe au Wine na nk, Vyakula hivi au Vinywaji hivi huwa na Madhara kwa Mama na Kichanga wake.
Unaweza kutembelea youtube channel ya @Dr.Mwanyika
Unaweza kusikiliza video yetu pale youtube.
Response to "Vyakula Muhimu Kwa Mama aliyejifungua kwa Upasuaji!"
Kwahy ili kula ugali na wali Mara kwa Mara Ni baada ya mda gani