Madhara ya MAINI na “VITAMIN A” kwa Mjamzito ni yapi?

Madhara ya MAINI na “VITAMIN A” kwa Mjamzito ni yapi?

Madhara ya MAINI na “VITAMIN A” kwa Mjamzito ni yapi?

Mojawapo ya Nyama pendwa kwa Wajawazito wengi ni nyama ya Maini inawezekana ni Maini ya Ng’ombe, Nguruwe, Mbuzi, Kondoo, Kuku, Bata na nk, Nyama ya Maini ya Wanyama mbalimbali huwa na kiwango kikubwa sana cha Vitamini A (Retinol), Matumizi makubwa ya Nyama hizo, Dawa au Vidonge vyenye Vitamini A nyingi huwa na Madhara makubwa kwa Ujauzito.

Tujifunze kidogo kuhusu Vitamini A;

Vitamini A (Retinol) na mazao yake (Retinoids) huwa na faida kubwa sana kwenye afya ya Mwanadamu ikiwemo kuhusika katika Kuona kwa Macho, Afya ya Uzazi ,Afya ya Ngozi, Nywele na Mifupa, Afya ya mwili na kuongeza Kinga ya Mwili kiujumla. Vitamini A imegawanyika katika Makundi makubwa manne (4) ambayo ni;

  1. Retinol aina hii ya Vitamini A hupatikana kiasilia na hutokana na Mazao ya Wanyama mfano: Nyama za Maini ya Wanyama,Maziwa ya Ng’ombe na Maziwa ya Mama anayenyonyesha.
  2. Retinal aina hii ya Vitamini A hupatikana baada ya Retinol kubadilishwa mwilini, ni zao la Retinol.
  3. Retinoic Acid aina hii ya Vitamini A ambayo huwa katika Mfumo wa Asidi hupatikana baada ya kubadilishwa kwa Retinal.
  4. β Carotene hii hupatikana kwenye baadhi ya Mimea yenye rangi ya Njano na Kijani mfano; Mboga za Majani, Karoti, Maboga, Viazi vitamu, na Matunda mfano; Maembe, Papai na nk,β carotene ambayo huweza kubadilishwa kwenye mwili wa Mwanadamu na kuzalisha kiwango kidogo cha Retinal ambayo ni aina mojawapo ya Vitamini A, lakini pia kuna aina nyinyine za Carotene kama α Carotene na β-cryptoxanthin .

JE MJAMZITO ANARUHUSIWA KUTUMIA VITAMINI A NA MAINI?

Jibu! Hapana Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), Mjamzito haruhusiwi kutumia Vidonge, Dawa au saplimenti za Vitamini A kama sehemu ya kliniki yake ya kawaida katika Ujauzito wake, ili kuepuka madhara yatokanayo na uwingi wa Vitamini A katika Mwili wa Mjamzito, Matumizi ya Vitamini A katika Kipindi cha Ujauzito bila kuruhusiwa na Daktari huwa na madhara makubwa kwa Mtoto aliyeko Tumboni.

WHO ina shauri ya kwamba;

  1. Hakuna ulazima wa Mjamzito kutumia Dawa au Supplimenti za Vitamini A katika kipindi cha Ujauzito, Una shauriwa kupunguza kiwango cha kutumia Vitamini A au kuacha kutumia Vitamini A unapokaribia kupata Ujauzito na kipindi chote cha Ujauzito.
  2. Wajawazito wanaoishi nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara mfano; Tanzania na nk sehemu ambazo kuna Wajawazito wengi wenye Upungufu wa Vitamini A, Wajawazito hao wanaweza kutumia kiwango kidogo sana cha Vitamini A ili kuepuka kutoona wakati wa Usiku au Giza, Kiwango cha (8000IU – 10000IU) kwa siku au 25000IU kwa Wiki na hutakiwa kuandikiwa na Daktari. Mwanamke ambaye alikuwa anatumia Vitamini A au Dawa za zenye Vitamini A nyingi hushauriwa asibebe Mimba angalau kwa Miezi 3 hadi Mwaka 1 tokea alipoacha kunywa Dawa hizo ili kuepuka madhara ya Vitamini A ambayo anaweza pata kama atakuwa na Ujauzito, Hivyo ni vema kutumia Uzazi wa Mpango wakati wa Matumizi ya Dawa zenye Vitamini A nyingi.

MADHARA NA ATHARI ZA MATUMIZI YA VITAMINI A NA MAINI KWA MJAMZITO

Mjamzito anayetumia Vitamini A au Vyakula vyenye vitamini A kwa wingi kwa mfano; Maini ya Ng’ombe, Mbuzi, Nguruwe, Kondoo au Maini ya Bata na Kuku, huweza kupelekea madhara na athari kubwa kwa Mtoto aliyeko Tumboni. Madhara hayo huweza kutokea pia endapo Mjamzito alitumia Vidonge vya Vitamini A au saplimenti hizo Mwanzoni mwa Ujauzito wake hususani kabla ya Ujauzito au kabla ya wiki 6 au 7 katika Miezi 3 ya Mwanzoni mwa Ujauzito kipindi ambacho kuna uumbwaji wa Kijusi au Mtoto aliyeko tumboni, Japokuwa matumizi ya Vitamini A hutakiwa kutumiwa kwa tahadhari au uangalifu sana Miezi 3 ya katikati na Miezi 3 ya mwishoni mwa Ujauzito au hata baada ya kujifungua kwa Mjamzito, Madhara ambayo Mjamzito anaweza kupata haswa kwa kiumbe chake kilichopo Tumboni ni kama;

  1. Mimba kuharibika ua kutoka kabla ya wiki 28 za Ujauzito
  2. Kujifungua Mtoto mwenye Udumavu wa Masikio.
  3. Kujifungua Mtoto mwenye Udumavu wa Taya la chini la Mdomo kuliko kawaida.
  4. Kujifungua Mtoto mwenye Mdomo wa Sungura.
  5. Kujifungua Mtoto mwenye udumavu wa Tezi ya Thymus ambayo huhusika kumpa kinga ya Mwili Mtoto mchanga.
  6. Kujifungua Mtoto mwenye Mgongo wazi au Ubongo wazi.
  7. Kujifungua Mtoto mwenye Magonjwa ya Moyo na shida katika mfumo wa Moyo.
  8. Kujifungua Mtoto mwenye Udumavu katika mfumo wa Fahamu na nk.

UMUHIMU WA VITAMINI A KWA MJAMZITO.

Pamoja na athari za Vitamini A kwa Mjamzito, bado Vitamini A ina umuhimu mkubwa sana katika Ujauzito hususani katika Ukuaji wa Mtoto aliyeko tumboni lakini pia na Mjamzito mwenyewe katika kipindi chote cha Ujauzito,Vitamini A huhitajika haswa Miezi mitatu ya mwishoni kipindi ambacho kunakuwa na Ukuaji zaidi wa Mtoto aliyeko tumboni mwa Mjamzito. Endapo Mjamzito atatumia Vitamini A katika kiwango stahiki kisichozidi 10000IU kwa siku au 25000IU kwa wiki hii huweza kuwa na faida kubwa haswa kwenye nchi ambazo kuna watu ambao wana upungufu wa Vitamini A mwilini mwao mfano; Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na Nchi za bara la Asia, Zifuatazo ni Faida za Matumizi ya Vitamini A kwa Mjamzito au katika kipindi cha Ujauzito endapo ikitumika kwa tahadhari kubwa na kiwango sahihi:

  1. Humsaidia Mjamzito kuwa na Afya ya Macho na kuongeza kuona haswa Muda wa Usiku.
  2. Humsaidia Mtoto aliyeko tumboni pia kuwa na afya nzuri ya Macho yake.
  3. Huongeza na kumjenga kinga ya Mwili ya Mtoto aliyeko tumboni.
  4. Huimarisha Mifupa ya Mtoto aliyeko tumboni na Mjamzito.
  5. Huimarisha afya ya Ngozi na Nywele za Mjamzito.
  6. Huimarisha Kinga na Afya mwili ya Mama Mjamzito.
  7. Huzuia na kumkinga Mtoto uwezekano wa Magonjwa ya Akili na Kisaikolojia kwa Mtoto mara baada ya Kuzaliwa.
  8. Humkinga Mjamzito dhidi ya Upungufu wa Damu katika kipindi cha Ujauzito.
  9. Husaidia Mjamzito kutojifungua kabla ya wakati au Mtoto kuzaliwa kabla ya wakati na nk.

MADHARA YA UPUNGUFU WA VITAMINI A KWA MJAMZITO.

Mjamzito huhitaji kiwango kikubwa zaidi cha Vitamini A ukilinganisha na Mwanamke ambaye si Mjamzito, hususani Mimba inapokuwa mwishoni au Miezi Mitatu ya Mwishoni mwa Ujauzito, kwa sababu ya ukuaji wa mtoto wake aliyeko tumboni ambaye huhitaji kiwango kikubwa cha Vitamini A katika Ukuaji wake. Mjamzito huhitaji kiwango kidogo sana cha Vitamini A haswa miezi mitatu ya Mwanzoni mwa Ujauzito hii ni kwa sababu Vitamini A huingiliana na Vinasaba vya mtoto na kuharibu ukuaji wa Mfumo wa Fahamu, Moyo na kusababisha udumavu wa baadhi ya sehemu za sura ya mtoto aliyeko tumboni.

Upungufu wa Vitamini A huweza kupelekea shida na changamoto nyingi kwa Mjamzito na Mtoto Mchanga ikiwemo;

  • Upofu wa Macho au Ukavu Macho kwa Mjamzito.
  • Udhaifu wa Mifupa kwa Mjamzito na Mtoto aliyeko Tumboni mwake.
  • Upungufu wa kinga ya Mjamzito na Mtoto aliyeko tumboni mwake.
  • Kushindwa kufanyika kwa Viungo Ipasavyo kwa Mtoto aliyeko tumboni.
  • Huweza kupelekea Upungufu wa Damu kwa Mjamzito.
  • Huweza kupelekea Mjamzito Kujifungua kabla ya wakati na nk.

VYANZO VYA VITAMINI A

  1. Vitamini A huweza kupatikana kiasilia kwenye Nyama za Maini ya Wanyama au Mazao ya wanyama mfano; Maziwa au Siagi, Samaki, Mafuta ya Samaki, Maziwa ya Mama anayenyonyesha, Vitamini A (Retinol) kutokana na Mazao ya Wanyama haswa Maini huwa ina Vitamini A nyingi sana ambazo huweza kuleta madhara makubwa kwa Mjamzito endapo akitumia mara kwa mara.
  2. Vile vile Vitamini A huweza kupatikana baada ya Mwili kuchakata β carotene zilizopo kwenye baadhi ya Mimea mfano: Mboga za Majani, Matunda mbalimbali, Karoti, Maboga, Papai na nk, Vitamini A kutokana na Mimea huwa ni chache zaidi na haiwezi kuleta madhara yoyote kwa Mjamzito.
  3. Vitamini A ambazo zimetengenezwa huwa zinaongezwa kwenye baadhi ya Vyakula kama Unga, Baadhi ya madawa, saplimenti na Vile huweza kutumika kama Vidonge au Dawa, Vitamini A zilizotengenezwa hutakiwa zitumike kwa tahadhari kubwa, WHO wanasema hakuna ulazima wa kutumia Vitamini A kama saplimenti kwa Mjamzito kwenye kliniki ya kawaida ya Ujauzito, Kama kuna ulazima,Basi haitakiwi kutumia kiwango kuzidi 10000IU kwa siku au 25000IU kwa wiki ili kuepuka madhara kwa Mtoto aliyeko tumboni kwa Mjamzito.

KUMBUKA: USHAURI MUHIMU KUTOKA KWA MAMA AFYA BORA

  1. Mjamzito usitumie Maini katika kipindi chote cha Ujauzito wako ni hatari kwa Afya ya Ujauzito na Mtoto aliyeko Tumboni, epuka haswa unapokaribia kubeba Ujauzito hadi Miezi 3 mwanzoni mwa Ujauzito
  2. Mjamzito usitumie Vitamini A kama hujaandikiwa na daktari vile vile hutakiwi kutumia zaidi ya 10000IU kwa siku au 25000IU kwa wiki hata kama umeandikiwa na Daktari.
  3. Ni vema kutumia Uzazi wa Mpango kama unatumia Dawa zenye Vitamini A nyingi kwa ajili ya kutibu magonjwa mengine mfano ; Magonjwa ya Ngozi.
  4. Kama una mpango wa kubeba Mimba basi subiri Miezi 3 hadi Mwaka 1 tokea uache kutumia Dawa zenye Vitamini A nyingi ili kuepuka athari za Vitamini A iliyopo mwilini katika Ujauzito wako.
  5. Tumia Vyakula vyenye Mimea ambayo ina β carotene ya kutosha bila wasiwasi wowote, katika kipindi chote cha Ujauzito haswa Miezi 3 ya mwishoni ya Ujauzito hakuna madhara yoyote hata ukitumia Mimea au Matunda hayo kwa Wingi kiasi gani ukilinganisha na Vitamini A kutoka kwenye Maini.

Response to "Madhara ya MAINI na “VITAMIN A” kwa Mjamzito ni yapi?"

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *