MIMBA KUHARIBIKA/KUTOKA MARA KWA MARA KUTOKANA NA UDHAIFU WA MLANGO WA UZAZI (CERVICAL INSUFFICIENCY)

MIMBA KUHARIBIKA/KUTOKA MARA KWA MARA KUTOKANA NA UDHAIFU WA MLANGO WA UZAZI (CERVICAL INSUFFICIENCY)

MIMBA KUHARIBIKA/KUTOKA MARA KWA MARA KUTOKANA NA UDHAIFU WA MLANGO WA UZAZI (CERVICAL INSUFFICIENCY)

UDHAIFU WA MLANGO WA UZAZI

Udhaifu wa Mlango wa Uzazi ni Hali au shida ambayo huhusisha Mlango wa Uzazi kushindwa kudhibiti au kuzuia Mimba isitoke mpaka kipindi ambacho Mtoto anakuwa amekomaa na tayari kwa ajili ya kuzaliwa au kwa kipindi Cha miezi 9 ya Ujauzito.

Hali hii huchangia asilimia 20 ya Mimba zote zinazoharibika katika Jamii.
Hali au Shida hii kitaalamu huitwa Cervical insufficiency wakati mwingine huitwa Cervical Incompetence.

Udhaifu wa Mlango wa Uzazi au Mlango wa Uzazi kushindwa kuendelea kufunga au kuweza kudhibiti Mtoto asitoke mpaka wakati ambapo Mtoto anakuwa amekomaa vizuri na kuwa tayari kuweza kuzaliwa huweza kupelekea Mjamzito kujifungua mapema zaidi pasipo kuhisi uchungu wowote, hii ni kwa sababu Mlango wa Uzazi huachia pasipo nguvu ya msukumo kutoka kwenye Mji wa Uzazi hususani katika Miezi mitatu ya katikati na Mara baada ya kujifungua Mtoto hufariki.

Je Hali au Tatizo Hilo husababishwa na Mambo gani?.
Tatizo hili au Shida hii Visababishi vyake  bado havijajulikana vizuri, japokuwa kitu chochote kile ambacho kinaweza kuhatarisha na kupelekea Mlango wa Uzazi kuwa dhaifu huweza kusababisha tatizo hili na madhara yake huwa ni kuharibika kwa Mimba Mara kwa Mara kutokana na Udhaifu wa Mlango wa Uzazi katika kipindi cha kati cha Ujauzito.

Je ni Mambo gani huweza kuhatarisha kupata Tatizo hili?
Mambo yafuatayo yanaweza kuhatarisha Mwanamke au Mama yoyote kuwa na Tatizo hili la kuwa na Mlango dhaifu usioweza kuhimili Ujauzito mpaka mwishoni mwa Ujauzito, Mambo hayo ni kama;

1. Mwanamke mwenye historia ya kupoteza au kuharibikiwa na Mimba Mara kwa Mara katika kipicha cha Kati cha Ujauzito kati ya wiki 14 hadi wiki 20.

2. Mwanamke mwenye Mlango wa Uzazi mfupi chini ya milimita 25 au sentimita 2.5 ambao umedhibitishwa na kipimo cha Ultrasound inayoingizwa ukeni.

3. Mwanamke mwenye historia yakujifungua Mtoto kabla ya wakati wa kujifungua katika Mimba zilizopita, Mfano kujifungua chini ya wiki 28 za Ujauzito.

4.  Mwanamke ambaye Mimba iliharibika na alifanyiwa Upasuaji uliohusisha kutanuliwa kwa Mlango wa Uzazi ili kuweza kusafishwa kutoka na mabaki ya uchafu Mara baada ya Mimba kuharibika.

5. Mwanamke aliyegundulika kuwa ana Udhaifu wa Mlango wa Uzazi katika Mimba zilizopita.

6. Kutolewa au kuondolewa kwa Tishu au kinyama kwa ajili ya utafiti au kama matibabu kwa mama ambae aligundulika ana Saratani ya shingo ya kizazi iliyoko katika hatua za mwanzo.

7. Kuumia au kuchanika kwa Mlango wa Uzazi kipindi ambapo Mama anapojifungua kwa njia ya kawaida au Ukeni ambapo huweza kupelekea Udhaifu wa Mlango wa Uzazi.

8. Upasuaji wa aina yoyote unaohusisha Mlango wa Uzazi huweza kupelekea kupata Udhaifu wa Mlango wa Uzazi.

9. Ulemavu wa Mji wa Uzazi na Mlango wa Uzazi kipindi ambacho Mwanamke apolikuwa anatengenezwa  Tumboni mwa mamaye, mfano : Mji wa Uzazi kugawanywa na Kuta moja katikati yake.

10. Kuzaliwa na Udhaifu wa Mlango wa Uzazi endapo mwanamke huyo alizaliwa kutoka kwa Mama aliyekuwa amewahi kumulikwa na mionzi fulani (DES).

11. Kuwa na Mimba ya zaidi ya Mtoto mmoja mfano; Mapacha au Watatu.

Je Dalili zipi nitazipata endapo nina Tatizo au Shida hii ya Mlango dhaifu?

Akina Mama wengi ambao wana Mlango dhaifu wa Uzazi huwa hawana Dalili zozote kipindi ambapo si Wajawazito au katika kipindi Cha Ujauzito hususani katika Miezi Mitatu ya mwanzoni mwa Ujauzito wao, Japokuwa baadhi ya Wajawazito huweza kuanza kuonesha au kuhisi dalili za Mlango dhaifu wa Uzazi kipindi cha Ujauzito Mimba inapofikisha wiki 14 hadi wiki 20, dalili hizo  ni kama;

1. Kuhisi Uzito kwenye kiuno au tishu zinataka kutoka kwenye sehemu za ukeni!

2. Maumivu ya kiunoni sehemu ya nyuma au maeneo ya Mgongoni karibia na kiuononi.

3. Maumivu ya kubana sehemu ya chini ya Tumbo.

4. Kutokwa na Damu kama matone matone.

5. Kutokwa na Maji ukeni endapo kama Chupa imepasuka.

Je Nitagundulikaje kuwa na Tatizo hili?

Kwa kawaida shida hii ya Udhaifu wa Mlango wa Uzazi kipindi Cha Ujauzito huwa si rahisi sana kuweza kugundulika kwa sababu huwa hakuna dalili au viashiria vya hali hii, japokuwa baadhi ya Wajawazito huwa na dalili tajwa hapo juu bado huwa changamoto kuweza kugunduliliwa na baadhi ya Madaktari au wahudumu wa Afya, endapo Mjamzito mwenye tatizo hili hakufanyiwa vipimo stahiki na kwa wakati au endapo hana historia ya kupoteza Mimba Mara mbili au zaidi.

Ili uweze kugundulika na shida hii unatakiwa kwanza uwe na historia ya kuharibikiwa na Mimba zaidi ya Mara mbili kipindi cha kati cha Ujauzito yaani Mimba kuharibika au kutoka pasipo kuwa na maumivu au Uchungu kati ya wiki 14 hadi wiki 20 na kujifungua Mtoto kabla ya wiki 28.

Vile vile unahitaji kufanyiwa Ultrasound ambayo hupitishwa katika njia ya Uke, endapo Mjamzito ana Udhaifu wa Mlango wa Uzazi Ultrasound itaoneaha njia ya Mlango wa Uzazi Kama herufi V au U au Y ambayo inakuwa imeanzia kutanukia kwa ndani ya mlango wa Uzazi na kuelekea nje ya Mlango wa Uzazi kuonesha kuwa Mlango huo ni dhaifu badala ya herufi T ambayo huonesha uimara wa Mlango wa Uzazi.

Pia ultrasound huweza kupima Urefu wa Mlango wa Uzazi kutoka kwenye tundu la ndani la Mlango wa Uzazi mpaka tundu la nje ambapo kwa kawaida huwa ni sentimita 2.5 au zaidi, endapo Urefu huo utakuwa chini ya sentimita 2.5 huonesha kuwa Mlango ni mfupi na huhatarisha Mlango wa Uzazi kuwa na Udhaifu.

Vile vile unaweza kufanyiwa uchungu kwa vitanuzi vya Mlango wa Uzazi katika kipindi ambacho si Mjamzito ambapo endapo kama kitanuzi kitaingia kwa urahisi huonesha Udhaifu wa Mlango wa Uzazi, tofuati na hapo huwa ni kinyume chake.

Je endapo nimegundulika na shida hii Matibabu yake huwa ni nini?

1. Matibabu ya shida hii ni kufanyiwa upasuaji wa kufunga Mlango wa Uzazi kwa kutumia nyuzi au utepe ili kuimarisha Mlango wa Uzazi, Upasuaji huu huweza kufanyika kuanzia wiki ya 13 hadi 14 ya Ujauzito ili kuhakikisha kwamba Mlango wa Uzazi kuhimiri kudhibiti kutoka kwa Mtoto mpaka atapokuwa amekomaa vizuri tayari kwa ajili ya kuzaliwa na kuweza kujitegemea katika Upumuaji na ukomavu wa mapafu.

Je Nyuzi au Utepe uliowekwa kipindi Cha Upasuaji wa kuimarisha Mlango wa Uzazi huondolewa lini ili kujifungua?

Baada ya kushonewa Mlango wa Uzazi ili kuimarisha Mlango wa Uzazi kwa ajili ya kudhibiti Mimba isiyoke, Utepe au Nyuzi huondolewa kuanzia wiki ya 36 hadi 37 kipindi ambacho Mtoto amekomaa vizuri na uchungu hauja anza, endapo uchungu ukianza unaweza kuharibu Mlango wa Uzazi uliofungwa na kusababisha hatari nyingi Sana kiafya ikiwemo kukatika kwa Mlango wa Uzazi.

2. Matibabu mengine ni matumizi sahihi ya Dawa ya Duphastone au Progesteroni ambazo hupunguza maumivu ya kubana na kuachia au nguvu ya mji wa Uzazi kumtoa Mtoto nje, vile vile hupunguza uwezekano wa kujifungua Watoto wadogo zaidi na wasio wakomavu, lakini pia endapo Mjamzito ana Mimba zaidi ya Mtoto mmoja haishauriwi sana kutumia Dawa za Progesterone, japokuwa huwa zina umuhimu mkubwa pia.

3. Unaweza kupewa Dawa za Madini Chuma kwa ajili ya kuhakikisha unakuwa na Damu ya kutosha na Vitamini mbalimbali ili kuimarisha Afya ya Mjamzito na Mtoto wake aliyepo Tumboni.

KUMBUKA: Hutakiwi kufanyiwa upasuaji na kufungwa Mlango wa Uzazi wako endapo una maambukizj ya vijidudu katika mfuko wa Uzazi au Mji wa Uzazi, Mimba kutishia kutoka au kujitokeza kwa Chupa kwenye mfereji wa Mlango wa Uzazi kutoka, Mlango wa Uzazi kuachia zaidi na  kutokwa na Damu au kuachia kwa Kondo la nyuma kujishikiza kwenye mji wa Uzazi na kutokwa na Damu.

Response to "MIMBA KUHARIBIKA/KUTOKA MARA KWA MARA KUTOKANA NA UDHAIFU WA MLANGO WA UZAZI (CERVICAL INSUFFICIENCY)"

  • Leave a Reply

    Your email address will not be published. Required fields are marked *